AuthorsDen.com   Join Free! | Login    
   Popular! Books, Stories, Articles, Poetry
Where Authors and Readers come together!

SIGNED BOOKS    AUTHORS    eBOOKS new!     BOOKS    STORIES    ARTICLES    POETRY    BLOGS    NEWS    EVENTS    VIDEOS    GOLD    SUCCESS    TESTIMONIALS

Featured Authors:  Odyssia Learning, iA.J. Mahari, iAnthony Dalton, iIolanthe Woulff, iWayne Anderson, iDavid Gelber, iErnie Heavin, i

  Home > Poetry > Books Popular: Books, Stories, Articles, Poetry     

Mwiti -o- M'Marete

· + Follow Me
· Contact Me
· Sponsor Me!
· Books
· Articles
· Poetry
· 5 Titles
· 1 Reviews
· Add to My Library
· Share with Friends!
·
Member Since: Aug, 2009

Mwiti -o- M'Marete, click here to update your pages on AuthorsDen.


Pepo Nne: Diwani ya Malenga wa Mlima Meru
by Mwiti -o- M'Marete   

Share this with your friends on FaceBook

Category: 

Poetry

Publisher:  Lulu.com ISBN-10:  0557132266 Type: 
Pages: 

132

Copyright:  2009 ISBN-13:  9780557132263
Fiction

Amazon
Lulu
Barnes & Noble.com
Lulu.com

An anthology of poems in Swahili based on everyday life. Themes include love and hate, politics, youth and parenting. Written -- strictly -- in the eons-old musical, rhymic style unique to Swahili poesy, it is suitable for general readers seeking recreation as well as scholars and students of, especially, Swahili literature.

“Pepo Nne” ni mkusanyiko wa mashairi sitini na sita yaliyogawanywa katika vifungu vinne: yaani Upepo wa Mapenzi, Upepo wa Vituko, Upepo wa Mafumbo, na Upepo wa Maisha.

Mithili pepo nne zivumazo angani, “pepo” hizi ni mchanganyiko wa hisia, matukio, wasia na ndoto za “Malenga wa Mlima Meru”.

Zikutanapo “pepo” hizi basi, hatima yake ni uhondo wa mantiki uliokaangiwa mafuta ya ustadi wa sanaa na kutiwa viungo vya maadili, mafunzo, vichekesho na maswala yenye kusisimua bongo la msomaji.

Alipoitunga diwani hii, mwandishi hakuwa akimlenga tu msomaji mwenye kutaka kukata kiu chake cha uraibu wa mashairi ya Kiswahili, au hata kutafakari juu ya maisha ya dunia ya leo, hasa kuhusu siasa, utu na dini. Diwani hii vilevile inaweza kutumiwa kufundishia mbinu za utunzi wa mashairi shuleni.

Kigaroni pamekwama swala nyeti la umalenga wa karne tuliyomo, na wasomi na wapenzi wengine wa fasihi hii wametoa maoni yanayohitilafiana kuhusu ni mashairi yapi yaliyo na hadhi ya juu zaidi. Yaani, iwapo ni yale yenye kuungama kikamilifu sheria za tangu jadi za utunzi wa mashairi ya Kiswahili - kama vile Pepo Nne - au yasiyojali kamwe sheria hizo, yaani free verse kwa kimombo, au, wayaitavyo wenye kuegemea ukae kama mwandishi wako 'mashairi guni'.

Excerpt
NIMPENDAYE MAMANGU
Nimpendaye mamangu, wengine siwathamini
Yu mwanzo na mwisho wangu, mapenzi ya mtimani
Kwani hanipi matungu, kwa mapenzi yaso shani.
Mama ’angu ndo hakika, kweli isobatilika
Ndiye asenipa shaka, dukuduku kadhalika

Kwake sitobabaika, kwa wema abubujika.
Pulika kwambie siri, ya mapenzi ya dhatiya
Japo uwile fakiri, kwa tabu moyo waliya
Ukisaka utajiri, mamako takufidiya.

Atakupa pumziko, na amani ya moyoni
Tabu kwako iwe mwiko, ujikute furahani
Likuishe babaiko, uridhike maishani.
Mama hatokukemeya, utendapo ya aibu

Bali takupa wosiya, wa dhati usoghilibu
Fikira hukutuziya, upumzike muhibu.
Mama wa mtu ni kitu, kumpuza ni haramu
Ingawa uwile jitu, kwake mithili sanamu

Bado u kisu kibutu, hujui tungu na tamu.
Tama napiga saluti, kwao wote kina mama
Heshima kwenu sharuti, wenu wana kuungama
Haipimiki kwa futi, nimpendavyo Mamangu.


PENDO LANGU
Sipendi wa kusikiza, niambavyo pendo langu
Chuki muwate ingiza, mharibu wimbo wangu
Wala msije puuza, sambe nishatiwa pingu
Malkia hushindiki, bara hadi maji male.

Nisikize kwa makini, sikuviki cha ukoka
Ndipomi nala yamini, moyoni hutonitoka
Enenda bara na pwani, juwa sitokutoroka
Warembo wangawa wangi, ndiwe nayenivutiya.

Matoyo huniangaza, kote nendako sione
Huwa nakufululiza, mwengine nisimuone
Hwendapo huomboleza, kasubiri tukutane
Mwengine sitotamani, ilawe pendoni mwangu.

Mwana uliyeumbika, kwa urembo hupitiki
Ni wangi wanokutaka, ela we hudanganyiki
Pendo sinipe talaka, mtoto msitahiki
Mwengine sitompenda, binadamu wala jini.

Magharibi matlai, kusini kaskazini
Mwengine sikubalii, nafasi yako moyoni
Na wala sikukimbii, nikakuata weleni
Pendo thama siniasi, tuishi tukipendana.


KHERI UPATE NAMBIYA
Kwa wangu alo moyoni, kiyangazi na masika
Nanena ya mtimani, bila ya kufedheheka
Pendo la tangu zamani, lipate kueleweka
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Ni wangu moyo waliya, ukinena ya mahaba
Mahaba kanivamiya, moyo wangu kuukaba
Hadi kanilazimiya, nifichuwe langu huba
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Sitaki uje ropoka, porojo ukazitiya
Habari sije ponyoka, waja wakatangaziya
Heshima ikanitoka, hadhi ukanishushiya
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Hino siri ni ya weye, usimwambie mwengine
Nataka weye na miye, asiwe kati mwengine
Ndiwe unipendezaye, hakuna mja mwengine
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Utulize wangu moyo, wahaka kuniondowa
Mawazo niliyo nayo, yanigeuza mtawa
Tiba nipa wako moyo, wala sitie madawa
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Uza hata na wa kale, ni lini wakati upi
Vitaze vishindikile, mahaba kwa mbinu zipi
Ni lipi lijile mbele, ya mahaba nena lipi?
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Mbona wanipa mashaka, ewe wangu wa moyoni
Na ndivyo nahangaika, huku nawe hunioni
Vichakani namulika, kajifita sikuoni
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

“Mhariri wa tabiya”, zako nimezihariri
Nionele zavutiya, nikazitiya muhuri
Nazo kanipendezeya, ndipo katunga shairi
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Nitabakiya weleni, japo unikataliye
Nikangiya mashakani, punguwani nibakiye
Taingiya ukatani, raha inipungukiye
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.

Nijibu pasi kusita, majibu upate tuma
Kabla mwiya kupita, raha yangu ikakoma
Nikachoshwa na kuteta, mtoni nikajitoma
Na kama nina kasoro, kheri upate nambiya.


DADA MZEMBE
Naliya dada mzembe, kwangu ajipendekeza
Kwa mashoka na majembe, kwangu ajisukumiza
Jinsi ‘livyo mbembe, kamwe sichi kumbeza
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Kwangu ajipendekeza, kwa fujo pasi kuchoka
Najaribu kumpuza, kabla kwangu kufika
Ela ninapomliza, ajaa huwa acheka
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Yu mzembe punguwani, sherati la “hai-teki”
Yu pumbavu “namba wani”, msiri piya “manoki”
Kumfuta aswilani, kwangu kamwe hafutiki
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Amejitiya matiko, afiya ja tembo-mwitu
Kanijaza mshituko, nikabakiya mbutu
Kunitiya sititiko, kuadhwibu wangu utu
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Alivyo na sura mbovu, ninabakiya kununa
Mkaidi na mvivu, katu sishi kusonona
Zitakuvundika mbavu, kiteko ukimuwona
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Onyo ndipo namuonya, toka leyo aniwate
Nambami ninamsonya, simi katu anipate
Ni mtungu kumung’unya, atanitema ja mate
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Dada saka kwengineko, kabla mwiya kupita
Kwani wanuka mnuko, na ushombo wa kutata
Simi sampuli yako, mtumba sitokufwata
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Sinione kifaranga, bado nachakura ghala
Miye dume la “manyanga”, siandami gulagula
Tausi mwenyi kuringa, kamwe sivili vya ghala
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.

Onyo usiposikiya, jinalo talitangaza
Halaiki kuwambiya, ndiwe ninayekubeza
Ubaki kuliyaliya, kwangu uwate jiuza
Huyuno dada mzembe, kwangu ajipendekeza.


NIMEPOKONYWA!
Haunishi mshituko, taharuki na sumbuko
Nikumbukapo vituko, kwa jonzi na sikitiko
Kanijiri ja maziko, kanijaza hangaiko
Nimepokonywa mpenzi, kwa mapesa darahima!

Japo nifanyile hima, chombo kisende mrama
Leo singenda jitoma, baharini nikazama
Ni mapesa darahima, alopewa kunihama
Nimepokonywa mpenzi, kwa mapesa darahima!

Aswili ya uswahiba, iwile ni ya haiba
Tupendanile kwa huba, tukawekana akiba
Ela ujile mswiba, mkwasi akambeba
Nimepokonywa mpenzi, kwa mapesa darahima!

Ali mwana mtulivu, aso mawi mazowevu
Likaja zee duduvu, lilalo mbichi na mbivu
Likamfanya muwovu, mlegevu mpotovu
Nimepokonywa mpenzi, kwa mapesa darahima!

Nami nilivyokereka, nimepanga mashitaka
Zee kortini tafika, jela lipate fungika
Kama mwezi utafika, mpenzi bado lamweka
Nimepokonywa mpenzi, kwa mapesa darahima!

Hili ni onyo onyeka, zee simi kuhiniwa
Kwani mwisho utamaka, adhwabu ikikufika
Takuzidiya mashaka, ubaki kusononeka
Nimepokonywa mpenzi, kwa mapesa darahima!

Meshawapasha habari, nawaata na kwaheri
Kwenye kina cha bahari, naregeya kwa saburi
Wamuzi nauahiri, dhidi hilino kafiri
Nimepokonywa mpenzi, kwa mapesa darahima!


NINGALIJUWA
’Penzi naumwa moyoni, na hivi vituko vyako
Kwani wanifinyiyani, hun’achii pumziko?
Asubuhi na jioni, wanipapasa mifuko!
Laiti ningalijuwa!

’Penzi sharuti nitete, moyo wanikereyani?
Huniruhusu nipate, wanisaka mifukoni
Mara “nipa” mara “lete”, ’Penzi huna shukurani
Laiti ningalijuwa!

Usingalikuwa wangu, awali ningalijuwa
Hata ukangiya kwangu, japo kuniamkuwa
Usingatafuna changu, japo kipande cha muwa!
Laiti ningalijuwa!

Umezidisha vituko, ukakiuka mipaka
Ajaa nala ukoko, huku unazo nafaka
Vitanda unavyo kwako, nilaliyapo mkeka!
Laiti ningalijuwa!

Hukuita “Penzi langu”, kwani n’na pendo kwako
Nawe ’menitiya pingu, nisijenda kwengineko
Dunia na pia mbingu, mwengine kuwa hayuko
Laiti ningalijuwa!

Yarabbi wangu Manani, nakuomba niokoe
Ewe Mola wa Mbinguni, dhiki yangu uitoe
N’epushiye hayawani, moyoni nami nipoe
Laiti ningalijuwa!


MBONA POTE NIFUMAPO...
Kulla ombi nitumalo, huwa ninatumaini
Ya kuwa niliombalo, ’tafanikisha Manani
Na kuwa nilikosalo, hukubali pasi soni
Mbona pote nifumapo, hatimaye nasonona?

Maombi niloyatuma, ja mtanga baharini
Kulla ninapolituma, haja yangu nisakini
Nami ninapolituma, huwa ni pasi utani
Mbona pote nifumapo, hatimaye ninakonda?

Lau manju nimesaki, sipenyi kutokezeya
Nalijidhani maliki, kumbe miye maoteya
Naliliya Mauluki, kukwama sijazoeya
Mbona pote nifumapo, hatimaye sikitiko?

Kuna yule “malkiya”, wa sura na matamshi
Kwake ndiko ‘kaanziya, hino kazi tatanishi
Lau ‘likotokomeya, bado kwangu ’na ubishi
Mbona pote nifumapo, hatimaye nateseka?

Halafu kuna kipusa, hajabaleghe mtoto
Kamwamba “Ewe Asusa, sitoweza mkeketo”
Kapuliza pasi kisa, kalihepa langu koto
Mbona pote nifumapo, hatimaye naumiya?

Akaja nae wa tatu, dosho liso mshindani
Ba’da ya myezi mitatu, h’onekani aswilani
Kumbe yule mtukutu, leo ni “Mama-Fulani?”
Mbona pote nifumapo, hatimaye jakamoyo?

Leo ninawamba hombo, hawano wavaa-rinda
Nionele mna kombo, mwengine sitompenda
Nimechoshwa na mashombo, yenu yamenikodesha
Mbona pote nifumapo, hatimaye mwaniliza?

Naapa sitothubutu, nimefika kikomoni
Ni kheri nishike kutu, “futa” lenu sitamani
Napiga mbizi ya kwetu, bahari kuu kinani
Mbona pote nifumapo, hatimaye dukuduku?


NIMTUKUWE, NIMWATE ?
Imenijiya takhshwishi, ndiposa situwi moyo
Dukuduku hazinishi, tangu jana hadi leyo
Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.
Sihiari aswilani, simwati tamtukuwa

Lau kuna ubishani, waja wananisumbuwa
Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.
Kuna mwana na mamaye, kwangu wanipa kisanga
Moyo wafanya niliye, kwa makuki wanidunga

Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.
Mwana ndiye nitakae, nia yangu nende nae
Daima niishi nae, nimlelee akue
Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.

Bali mvyele kumwata, kunradhi taridhika
N’ona atakuwa tata, nishi ninahangaika
Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.
Lau pana masharuti, mmoya simtukuwe

Pia mmoya simwati, sharuti pamoya wawe
Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.
Ndiposa nakuna kitwa, nimeshindwa nitendeni
Kabula kufanya fatwa, kwa hasidi na mwendani

Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.
Tama nituzani moyo, nipowe naungulika
Wala msone uchoyo, muniate kuteseka
Mzito hatukuliki, na kumwata sihiari.


NALINDA YANGU ASALI *
Miye nyuki mwenyi choyo, nalinda mzinga wangu
Niupendao kwa moyo, nikaujengeya dungu
Ndipo wadoezi doyo, kwangu waona utungu
Miye nyuki mwenyi choyo, nalinda yangu asali.

Ni asali ya thamani, nadra hipatikani
Ulaya na Marekani, Urusi na Ujapani
Hutopata aswilani, bali ya thamani duni
Nalinda yangu asali, waja wasiinyakuwe.

Hino asali fadhili, daima yaniongowa
Tamu kushinda kubuli, kwa sifa hijapunguwa
Nd’o katu siendi mbali, isije ikaibiwa
Nalinda yangu asali, waja wasije doweya.

Ni nyuki na asaliye, siwataki wadowezi
Kwangu msikaribiye, wanyang’anyi na majizi
Nawe unipuuzaye, ole kwa wako uzozi!
Nalinda yangu asali, waja wasiibugiye.

We asali yangu tuwa, uzidishe na utamu
Ule wako wa muruwa, hadi nitapozuumu
Kukuonja kwa hatuwa, kuchovyachovya kwa zamu
Nalinda yangu asali, waja wasije iramba.

Daima nitakulinda, hatiya isikufike
Wezi wanaokuwinda, ulipo wasipafike
Kusudi nafanya inda, nd’o moyoni uridhike
Nalinda yangu asali, waja wasije ionja.

Tamati natiya doti, kisa nyuki na asali
Asali hamuipati, enyi wezi wa awali
Kwani nimeidhibiti, leyo na mwiya tawili
Nalinda yangu asali, kwa mikuki yenye moto.

* Shairi hili lilitunukiwa tuzo la “Shairi la Wiki”
kwenye gazeti la Taifa Leo.


MUHIBU NATAKA TWIBA
Nakutuma na salamu, njiwa kwa wangu muhibu
Kwani moyo nina ghamu, tangu aliponighibu
Akili sina timamu, na ndiye wa kunitwibu
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.

Moyo nami sijihali, njozi zimenizidia
Nami usiku silali, kucha namfikiria
Piya sinywi wala sili, pendole lanisumbua
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.

Nimekua punguwani, si hayati si mamati
Najisemesha ndiyani, ja aso bongo thabiti
Lau bado ni makini, pendo nimelizatiti
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.

Daima ninamuwaza, hanitoki mtimani
Pendole lanitatiza, sifaze nikizighani
Jinsi ’navyopendeza, kwa umbole lenyi shani
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.

Mwambie afanye hima, aje atende wajibu
Aniongowe mtima, kabla sijawa bubu
Moyo uwate niuma, pendo lilonisulubu
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.

Mwambe akiahirisha, safari kutoifunga
Ari yangu ikanisha, kabla hajanipunga
Nami kesho sitokesha, usiku nitajinyonga
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.

Umwambe sikisinidi, kisa hichi cha mswiba
Lau ni yangu fuadi, yaliya yataka twiba
Ndiye peke tanifidi, ajapo nipa mahaba
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.

Tama najibwaga tini, nibaki nagaagaa
Hadi anipe idhini, nipone kutojifia
Mwambe afanye imani, aje na twiba murua
Njiwa peleka salamu, mwambie aje haraka.


NG’OMBE MNYAMA PUMBAVU
Kuranda kuku na kule, waja sijona lengine
Bara hadi maji male, panya hata tembo nene
Pumbavu kiasi kile, lilimalo lisivune
Sijona nyama pumbavu, kupita hilino ng’ombe.

Kupita hilino ng’ombe, sijona nyama pumbavu
We lipe chumvi lirambe, hadi lijikune mbavu
Na zizile ulipambe, ulizingire kwa wavu
Sijona nyama pumbavu, kupita hilino ng’ombe.

Asubuhi na mapema, hurauka nyama hili
Kula nyasi siku nzima, jengine huwa muhali
Uwandani tajitoma, majangaye kuhimili
Sijona nyama pumbavu, kupita hilino ng’ombe.

Kwenyi mbung’o waumao, litashinda nyama hili
Na nzi watatizao, mbu wasotajamali
Piya mani yadungao, haya yote lahimili
Sijona nyama pumbavu, kupita hilino ng’ombe.

Kuwe pepo maleleji, kimbunga na kiyangazi
Mwavuli lingahitaji, laula si lake ngozi
Lazidisha na ulaji, halina nyengine kazi
Sijona nyama pumbavu, kupita hilino ng’ombe.

Basi ijapo jioni, jua lendapo makazi
Ng’ombe hungizwa zizini, kukamwa pasi ajizi
Maziwa yote ziwani, hutowa pasi ushuzi
Sijona nyama pumbavu, kupita hilino ng’ombe.

Mngamba kuna pumbavu, kupita hilino nyama
Lau muwe wapotovu, akili zarudi nyuma
Japo mna wazo pevu, nambeni pasi tuhuma
Sijona nyama pumbavu, kupita hilino ng’ombe.


CHA MRUNGURA
Nifanyile utafiti, kwa walaji mrungura
Nikajuwa hawaketi, na kuifanya subira
Huwa kite ja banati, aogopaye tohara
Ni vipi cha mrungura, hakiketi mfukoni?

Ulapo cha mrungura, maelfu milioni
Bado huwa wazurura, hutuwi mwako moyoni
Waparura wakwangura, daima u hasirani
Ni vipi cha mrungura, hakiketi kikatuwa?

Upokeyapo kwa huno, mkono hupita “fwii!”
Kitwacho ukune kuno, ulile ukala mbii
Moyo ukaguna guno, kwenye waja hutulii
Ni vipi cha mrungura, hakiketi kikapowa?

Rushwa upawapo hongo, japo tamu ja mafuta
Takuja vundika gongo, maafa ukayapata
Matoyo yakawa tongo, kwako giza liwe tata
Ni vipi cha mrungura, hakiketi kufaidi?

Nipani jibu makini, wa bara na maji male
Nijuwe chake kiini, japo hadithi ya kale
Lishe kuniuma ini, ninafa jama simile!
Ni vipi cha mrungura, hakiketi kikakaa?

Ninakuita Ba-Chombo, nijibu pasi kusita
Na wa Taveta Luwambo, ndugu Muthomi natweta
Namudyero fanya lumbo, na Kigungwa msi vita
Ni vipi cha mrungura, hakiketi kikalika?

Wababa sikusahau, Amina na Joka Kuu
Kwa methali na nahau, nitibu ugonjwa huu
Karani sinisahau, katika mkasa huu
Ni vipi cha mrungura, hakiketi ja cha haki?

Tamati cha mrungura, jaani ndipo makao
Enenda ukachakura, mrandaji msi kwao
Lau manju sili kara, walaji wapo wa tao
Ni vipi cha mrungura, hakikai mfukoni?


UPI UGONJWA MBAYA?
Upi ugonjwa mbaya, unaoshinda wa njaa
Hilino lanipumbaya, suwala lanisumbua
Ndiposa nauliziya, jawabu nasubiria
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?

Njaa yauma matumbo, na kuyatiya madonda
Manju nishindwe malumbo, hadi hatima kukonda
Nisichambuwe mafumbo, ngomani siwezi enda
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?

Ndwele hino ndwele mbii, ndwele isopata tiba
Hijuwi mwema na mui, mahubiri na hotuba
Majabari haijui, madubwana na mibaba
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?

Hata Ukimwi mwuaji, ni afadhali kwa njaa
Kwani hauguwi Haji, danguroni asongia
Ela hata uwe jaji, njaa hutoikingia
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?

Yanipatapo mahoma, matembe nitamezeya
Aula uwe ukoma, tabibu kushitakiya
Lau njaa nalalama, tata yanitatiziya
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?

Rabbi nijaliye duwa, njaa kuniepushiya
Unipe yalo muruwa, ma’kuli ya kudoneya
Uwe uji au miwa, wali sitobaguliya
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?

Nataka yule tabibu, mjuzi wa mbii ndwezi
Ambe dawa ya kutibu, njaa na yake mizizi
Waja waate ghilibu, tiba wakiimaizi
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?

Tama najitoma ndani, baharini nikafie
Ninaumwa matumboni, Rabbuka nihurumie
Ninakhofu kigaroni, hwenda Manju niotee
Upi ugonjwa mbaya, kuzidi ule wa njaa?


SIMI
Simi koma kunitaja, unapowahadithiya
Uwadanganyapo waja, kwa Mola kushitakiya
Kwamba ndimi niso tija, mawi nimekutendeya
Eti naona faraja, mambo yakikulemeya
Tena ninao mrija, sumu kukunyunyiziya
Simi nikupele wembe, un’okukata maini!


MCHAMA AGO HANYELE*
Asalamu alekumu, na mjaliwe na kheri
Na baraka za Rahimu, mlisomapo shairi
Liso ma’tiki adimu, hilino nalikariri
Funguweni masikizi, maozi ’sibwage tini.

Dhamira ya kuandika, shairi pasi kusita
Muradi mkaonyeka, shairi mkilipata
Naomba watapulika, waja ma’na kuipata
Ni tungo lilo adili, methali nafafanuwa.

Methali ina asili, ya lahaja mojawapo
Ni katika Kiswahili, cha jadi ilokuwapo
Lilobaki kujadili, ni maana iliyopo
“Mchama ago hanyele, hwenda akauya papo”.

Wanenele wa awali, wakale walokuwepo
Ma’na yake ya asili, na wakati uliopo
Msafiri hachafuli, popote ashukiyapo
Kwani hwenda karejeya, karudiya papo hapo.

Maana yake ya ndani, yapatikana viwazi
Imechorwa kwa launi, isiyo na pingamizi
Nawafafanuliyeni, wasoweza kumaizi
“Mchama ago hanyele, hwenda akauya papo.”

Unapotuwa pahali, maskani yasodumu
Mwisho tapanda jamali, na kwenda mastakimu
Waja watakujadili, uendako kwa kudumu
Jinalo watalichora, kwa tabiya waloona.

Kwa tabiya waloona, ndivyo watakukumbuka
Japo wali wa kunena, kusengenya kadhalika
Ama wa kutukanana, viumbe wakaudhika
Jina lako kulitaja, ni haramu mutlaki.

Na japo uwile jizi, wengine kuwaibiya
Ujuvi na udakuzi, ubazazi kufwatiya
Au ukawa ajizi, kuchelewa kuzoeya
Waja watakukumbuka, midomo waitafuna.

Nawatoleya wasiya, maadui kwa muhibu
Walo na hino tabiya, waijuwe ni aibu
Kwani waweza rejeya, kule ulipoghilibu
Waja wakakukumbuka, kwa hasira na hamaki.

*Shairi hili ndilo lililokuwa la kwanza la mwandishi kuchapishwa
gazetini, kwenye Taifa Leo, mnamo 1987.


NYANI AONE KUNDULE
Funguweni masikizi, mupate yangu sikiya
Ninenayo mumaizi, kesho musije kuliya
Naeleza waziwazi, musije kosa sikiya
Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

Ni wa kale wanenele, katu haiwezekani
Bara hadi maji male, mbinguni na duniani
Nyani haoni kundule, hata kwa Kudura ipi
Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

Ela itawezekana, japo shime akitiya
Apate kuzindukana, kwa mizani kujitiya
Uzito wake kuona, bila tu kwa kukisiya
Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

Leo sikizi funguwa, hilino suwala tata
Fanya hima kwiyelewa, kesho usije kujuta
Nafusiyo kuelewa, kabula mwiya kupita
Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

Hata uwe jamadari, na tiara bega zima
Usipo jitahadhari, “cheni” usimame wima
Uizidishe fahari, ja aloumbwa kwa chuma
Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

Chunga unaposimama, kaguwa wako msingi
Chunga usije terema, ukabiringa “biringi!”
Jigange panapouma, japo mganga hagangi
Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

Hata uwe profesa, wajuwa duniya nzima
Ama ni mwenyi mapesa, manoti ni chungu nzima
Au mrembo kipusa, popote twakutazama
Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.

Usinite mnafiki, kunirushiya matusi
Lau japo hutosheki, usijawe wasiwasi
Mbona kalamu hushiki, pamoya na karatasi?

Na uwe mwamko mpya, nyani aone kundule.


UREMBO SI SHANI
Malenga nisiye shari, natowa wangu mliyo
Niwausiye ya kheri, kwa mambo niyaonayo
Lau kamwe siaziri, msiniwiye uchoyo
Urembo hauwi nde, funguwa wingiye ndani.

Zinduka usingizini, sikiya wangu wasiya
Uweke wako moyoni, ujuwe nimekwambiya
Kweli uzuri si shani, uzuri ni wa tabiya
Urembo hauwi nde, funguwa wingiye ndani.

Manani alikuumba, na kwa wingi ustadi
Akakujenga ja nyumba, uzuri uso utadi
Kakujengeya kirimba, ndiposa usikatadi
Urembo hauwi nde, funguwa wingiye ndani.

Nne naenda likizo, nikisubiri maoni
Tuitiliye mkazo, tabiya njema jamani
Tabiya njema nd’o nguzo, ya urembo siyo shani
Urembo hauwi nde, funguwa wingiye ndani.


MANANI HANAYO MASA
Kwa kishindo na mliyo, najibwaga kigaroni
Niweleze nilo nayo, pasina kuwafitini
Siwatii jakamoyo, wala sambi ya utani
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu.

Waja nd’o wajidhulumu, kwa kujitendeya mai
Manani kumlaumu, juwa kamwe haifai
Kwani siku ya Hukumu, hwenda ukapewa mbii
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu.

Binadamu hujitapa, kujifanya “namba wani”
Hujidai ndiye papa, unyongewe haunoni
Na kuranda akiapa, hashindiki aswilani
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu.

Utamuwona tajiri, mali aozesha kwake
Mali madal-bassari, ufukara ndoto kwake
Akajiona hodari, kuwanyanyasa wenzake
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu.

Tangi kwake nd’o sahani, atumiayo kulia
Maskini aswilani, hampi na masalia
Atayamwaya jaani, fukara waje fukua
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu.

Hebu jaribu ndu’yangu, muombe shilingi tano
Ataliya kwa utungu, akusimuliye ngano
Aape hata kwa Mungu,’kiuma chanda kwa meno
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu.

Mola ’tapokasirika, amfanye maskini
Moyo utamchafuka, amlaumu Manani
Matusi yatamtoka, machafu yaso kifani
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu .

Kama angesaidiya, fukara mwenyi taabu
Mola akamliliya, dhambi zake akatubu
Shida ’singemfikiya, angepata matibabu
Manani hanayo masa, waja nd’o wajidhulumu.


USHUZI ULOUJAMBA …?
Ushuzi ulotandika, ndugu sikunjiye puwa
Ukajifanya kumaka, samahani ukapawa
Mja ukahuzunika, mithili ya alofiwa
Ushuzi uloujamba, puwa waikunjiyani?

Waikunjiyani puwa, na kumbe ndiwe aswili
Udaku ulidakuwa, tukashindwa kuhimili
Ukajifanya mjuwa, waja wasikukejeli
Ushuzi uloujamba, puwa waikunjiyani?

Kamwe sitokusitiri, kukoma usipokoma
Kujifurisha kidari, kujidai mwenyi ngoma
Kuwarukiya mahiri, kuwafanyiya shutuma
Ushuzi uloujamba, puwa waikunjiyani?

Kibwebwe wajifunganya, na kujifanya Imamu
Malenga wawasengenya, kwamba ni waso timamu
Kumbe wausaka mwanya, unyiye mastakwimu
Ushuzi uloujamba, puwa waikunjiyani?

Kulla siku kigaroni, wafurisha matukano
Ushajileta weleni, ndiwe mwenyi farakano
Kumbe ndiwe majununi, mawele wacheka ngano
Ushuzi uloujamba, puwa waikunjiyani?

Bure kujifanya “seti”, eti u Kadhi Mkuu
Ukawapima kwa futi, wenziwo kuwanukuu!
U kibanda cha makuti, kidebe kikuukuu
Ushuzi uloujamba, puwa waikunjiyani?

Mesha ya kukukosowa, Manju nenda piga mbizi
Usite kutuzuzuwa, kwa mambo tusomaizi
Ya mnuko kukohowa, kutushutia mashuzi
Ushuzi uloujamba, puwa waikunjiyani?


TEMBO SI HUJA
Ndugu pokeya waraka, uusome ufahamu
Kabula mwiya kufika, ukazongwa nayo ghamu
Kuzingirwa na gharika, Mola ukamshutumu
Si huja lilivyo tamu, tembo huleta zahama.

Tembo huleta zahama, si mno lilivyo tamu
Kulipata ni gharama, utalipa darahimu
Ba’daye ’takuja guma, ja jibwa lenyi mizimu
Si huja lilivyo ghali, tembo huleta zahama.

Huleta zahama chupa, unapo kuizoweya
Jamaa utaitupa, mitaani kurandiya
Mithili fisi wa pupa, nyute kukudondokeya
Si huja lilivyo raha, tembo huleta zahama.

Si huja wala si mno, tembo lakufurahisha
Kukuweka roho nono, hakuna cha kukutisha
Litaleta malizano, raha yendapo kuisha
Si huja ulisifuvyo, tembo huleta zahama.

Linaleta masumbuko, mtimao kusumbuwa
Ngoja uje mlipuko, tembo likakuzuzuwa
Ja punda mteremko, kasi ukaitimuwa
Si huja tembo si mno, tembo huleta zahama.

Sahibu takutoroka, mambo yendapo mrama
Ulipo wabingirika, toka juu ya mlima
Huku ushafilisika, mahasidi wakusema
Si huja linavyonywewa, tembo huleta zahama.

Malumbo nafika tama, uyameze uyateme
Uwe mtimba kisima, au mshika umeme
Ndiwe na wako mtima, ukae ama uhame
Ela nanena si huja, tembo huleta zahama.


MUWATE AJICHAMBUWE
Wakongwe hata wavyele, wasiya upulikani
Nanena yano wapule, muyatiye akilini
Ndimi mlumbi wa kale, nanyi msinipuzeni
Muwate ajichambuwe, mwana awe atakacho.

Mwana simfanye yai, umpike utakavyo
Umuuwe ali hai, jinsi ’mwangamizavyo
Shurutizo hazifai, eti awe umwambavyo
Muwate ajichambuwe, mwana awe atakacho.

Awe kile atakacho, ajimudu maishani
Usimwangaziye macho, umtiye taabuni
Hujuwi faida yacho, kisomo chake makini
Muwate ajichambuwe, mwana awe atakacho.

Bure wavimba mashavu, sharuti awe karani
Au mwalimu shupavu, eti wakili makini
Bure wajipa uchovu, ’kwambiavyo si utani
Muwate ajichambuwe, mwana awe atakacho.

Usambe awe rubani, aula mkurugenzi
Ama hakimu kortini, eti awe mkufunzi
Shahada wampeyani, bado ali mwanagenzi?
Muwate ajichambuwe, mwana awe atakacho.

Ningambwa niwe twabibu, mwashi au seremala
Bure ningajipa ta’bu, hatima sumu kuila
Ningateseka muhibu, mumake mkiniola
Muwate ajichambuwe, mwana awe atakacho.

Kaditamati malumbo, naregea baharini
Nilolumba yasi kombo, muyawaze kwa makini
Muukomeshe ushombo, musite upunguwani
Muwate ajichambuwe, mwana awe atakacho.


SITOKESHA KWENYE NGOMA
Manju nafanya tambiko, mbali kupungiya mwiko
Ulonipa sikitiko, nikaudhika udhiko
Mwisho ukaja mwamko, nyani k’ona kundu liko
Ndiposa sikeshi tena, kwenye ngoma mdundiko.

Kwenye ngoma mdundiko, si mimi tena kuwako
Kusakata sakatiko, kukatika mkatiko
Wala kucha mdundiko, simi kwenye rukoruko
Simi wa kukesha tena, kwenye ngoma mdundiko.

Simi ngomani kuweko, katu hunipati huko
Hata unuse nusiko, wajisumbuwa sumbuko
Limenitosha ridhiko, nikapanga pumziko
Simi wa kukesha tena, kwenye ngoma mdundiko.

Tangu jana ningaliko, natingisha tingishiko
Katimiza mualiko, kuitika muitiko
Hadi kwenye kusanyiko, kutimiza timiziko
Simi wa kukesha tena, kwenye ngoma mdundiko.

Ni uchovu ulioko, badili ya mridhiko
Nasonona sononeko, kwa majuto yaliyoko
Najuta ’singekuweko, kwenye ngoma sokomoko
Simi wa kukesha tena, kwenye ngoma mdundiko.

Nalifunika funiko, lumbo lino la vituko
Nisikereke kereko, kuchafuka mchafuko
Tena sitaki mwaliko, gizani mithili fuko
Simi wa kukesha tena, kwenye ngoma mdundiko.


NDWEZI
Nina ndwezi, mbii isiyotibika
Sijiwezi, silali nikarauka
Haikomi!

Mlo sili, hivi miye nafa njaa
Pilipili, na asali ni sawia
Kumezeka ni muhali!

Najikuna, ni ja nateza gitaa
Nasonona, kwa hino ndwezi ajaa
Hainishi!

’Na uvimbe, kulla pahala kuvimba
Nawe sambe, ya haramu nimeramba
Iniveme!

Nawasihi, sala mtowe nipone
I ghabihi, hino ndwezi tata nene
Nateseka!

Ewe Mola, Rabi nijaliya duwa
Hino sala, nakutoleya Moliwa
Niponyeke!

Tama ndwezi, Inshallah taniondoka
Kwa mizizi, ing’oke na kukauka
Ninawiri!


WARINGIA NANI?
Manju ninayo huzuni, mambo ninayoyaona
Yakifanywa na fulani, urongo uso bayana
Nauza twaringiyani, nasi tu waja wanyonge?

Ola linavyojitapa, jibaba lijihisivyo
Linadhani ndilo papa, jinsi lijisifuvyo
Baba waringiya nani, na urithi kaachiwa?

Kaka naye yu papale, ajihisi ndiye “seti”
Na jinsi aringile, kupeperusha manoti
Kaka waringiya nani, na pesa za “omba-omba”?

Dada naye simuwati, ajihisi malkiya
Adhani ndiye “simati”, hana wa kumfikiya
Dada waringiya nani, na mavazi ya mtumba?

Mama hakuatwa nyuma, ndo mjuzi wa kuringa
Nyaka arudisha nyuma, na kujifanya “manyanga”
Mama waringiya nani, mvi unazo kitwani?

Muole mwanasiasa, huyuno Mheshimiwa
Leo ashakuwa tasa, akaitwa “mwizi-miwa” !
Mwanasiasa waringa, na kura za kughilibu?

Mwalimu aliya bwata, ndiye msomi halisi
Kumbe tabu yamfwata, atimuwa ja farasi!
Mwalimu waringiyani, na bado hujahitimu?

Karani ata maringo, bure waringiya waja
Taufikia ukingo, mashuzi yakikuvuja
Karani waringiyani, na vyeti vya kughilibu?

Nawe “askari-kanga”, wajihisi ndiwe mwisho
Kwa pingu unawafunga, waso masa kwa vitisho
Afisa waringiyani, nayo hongo ya kuhongwa?

Mangi ningaliyanena, mwiya ndiwo wanitata
Nawasihi hadharina, maringo tupate ata
Malenga waringiyani, na tungo za kuigiza?


MSINGELIJENGA KUTA
Wambile zama wahenga, kuhusu kuta na nyufa
Eti kuta mngejenga, na kuzipuuza nyufa
Nanyi kando kajitenga, ndiposa kuna maafa
Msingelijenga kuta, hamngeziziba nyufa!

Ola zilivyoko nene, nyufa zilivyopanuka
Zawafanya msonone, akili zishawaruka
Ramli na manemane, si mno masakasaka
Msingelijenga kuta, hamngeziziba nyufa!

Si mno ’livyo khatwari, mno asiliye nyufa
Hizino nyufa za mbari, ukabila utaifa
Zilizowapa kiburi, mwapigana hadi kufa
Msingelijenga kuta, hamngeziziba nyufa!

Mno zino kuta nene, mlozijenga awali
Hizo zenye mbii sine, ja Mnara wa Babeli
Mkaapa pande nne, mja kembe hatawali
Msingelijenga kuta, hamngeziziba nyufa!

Leo kuta zina nyufa, mzibi zikazibika
Wanyama na waja wafa, kote kote ni gharika
Ola yatangaa mafa, damu yafanza masika
Msingelijenga kuta, hamngeziziba nyufa!

Enyi bomoweni kuta, hizino za takhshwishi
Mwambe zino kuta mata, la sivyo janga halishi
Nami sishi kuwasuta, sikhofu wenyu ubishi
Msingelijenga kuta, hamngeziziba nyufa!


UKIMWI DUDU AJAA
Kuzukile dudu geni, kati ya wana Adamu
Umbile ni ja kunguni, waja lawafyonza damu
Kulitowa duniyani, pasi Kudura vigumu
Kuzukile dudu geni, UKIMWI ndilo jinale.

UKIMWI ndilo jinale, hilino dudu ajaa
Halijuwi wateule, wote linawasongoa
Bara hadi maji male, lino dudu katangaa
UKIMWI dudu ajaa, limeyaasi madawa.

Limeyaasi madawa, bure ungayanyunyiza
Matataye na beluwa, usije kuyapuuza
Kwani utalaaniwa, dudu ukilipiliza
UKIMWI dudu ajaa, lafyonza pasi huruma.

Lafyonza pasi huruma, gogo libaki kijiti
Mara linapokuuma, hakikaye ni mauti
Wendapo warudi nyuma, huna akili thabiti
UKIMWI dudu ajaa, hima tulipige vita.

Hima tulipige vita, hilino dudu haramu
Lipigwe bomu na mota, amri liisalimu
Shime twende likamata, lino dudu lenyi sumu
UKIMWI dudu ajaa, lakwepa likiviziya.

Lakwepa likiviziya, hilino dudu tukutu
Juwa linapokungiya, damuyo mengiya kutu
Dukuduku kukutiya, kiwewe pia mautu
UKIMWI dudu ajaa, langiya kwa nyingi njiya.

Langiya kwa nyingi njiya, kwanza mapenzi haramu
Na damu iso dhatiya, na wazazi wenye sumu
Pale ukajikondeya, ishapitishwa hukumu
UKIMWI dudu ajaa, limeyaasi madawa.

Limeyaasi madawa, ya wadudu na magugu
Waja limetushituwa, jidudu liwile sugu!
Lichunge dudu lauwa, mithiliye donda-ndugu
UKIMWI dudu ajaa, chunga lisije kuuma.


UNAHODHA HUUWEZI
Kuna nahodha mmoya, duni hajawa jagina
Ndiposa namuusiya, hapano kwa hadhwarina
Kwani pote ’kipitiya, abiriya wanaguna
Unahodha huuwezi, wang’ang’aniya sukani!

Wajitiya hamnazo, eti nahodha hodari
Kumbe umeoza ozo, mashombo umesitiri
Umegeuka kigezo, kilichovikwa jabiri
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.

Rudisha chombo haraka, upeane usukani
Abiriya wana shaka, wanakhofu safarini
Unawatiya dhihaka, kung’ang’aniya sukani
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.

Abiriya wanateta, chombo kinayumbayumba
Nawe huku unajeta, imekujaa kasumba
Safari unayotaka, khatwari itawakumba
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.

Umezoeya tulivu, isochafuka bahari
Bado hujawa mpevu, wajifanya u mahiri
Donda u mteka kovu, u watezeya bahari
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.

Leyo imeshachafuka, bahari haipendezi
Nawe hujamakinika, kuikabili huwezi
Wang’ang’ana unajika, japo hunacho kinyezi
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.

Mna nyangumi na papa, baharini mwanagenzi
Bure hapano watapa, utajageuzwa gunzi
Sikila hombo nakupa, uwate wako ushenzi
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.

Usiteze na bahari, tangu leo nisikiya
Ondowa chako kiburi, bure utaangamiya
Miye manju msi shari, mkasa nakwondosheya
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.

Dharuba nd’o hino yaja, nakupa onyo la mwisho
Sisi hatutoingoja, tukaja zama zamisho
Uhai kwako si hoja, tosha nd’o huno mlisho!
Unahodha huuwezi, rudisha chombo haraka.


FUNDI MTIMBA MALINDI
Fundi mtimba malindi, ndanimwe moya watapa
Wendo litimbiya lindi, ndanimwe uje watupa
Leyo umetomwa dindi, mjeuri mwenyi pupa
Fundi mtimba malindi, mbona tozi lakutona?

Uufanyile ushenzi, upoyatimba malindi
Kwani kasahau gunzi, awali liwile hindi
Lau weye mwanagenzi, wajisifiya ufundi!
Fundi mtimba malindi, mbona leo wasonona?

Ungalitimba malindi, ya katiti na ya kina
Tungajuwa weye fundi, mtimba-lindi jagina
Hungalinatwa na gundi, ukawa leo waguna
Fundi mtimba malindi, mbona leo u wajuta?

Awaye fundi hodari, yule aliyetimiya
Asotimba ya dosari, moya akatumbukiya
Hatimbi ja kitimiri, chuki akizingatiya
Fundi mtimba malindi, nambe chakuliza nini?

Ndiwe mtimba malindi, katimba yote ya kina
Hukuvitimba vilindi, katiti viso vya kina
Ndiposa liyapo kundi, wangine wapate pona
Fundi mtimba malindi, ndanimwe leo waoza!

Hukudhani tafukuzwa, welekezwe malindini
Jinsi ’livyotukuzwa, eti ndiwe “namba wani”
Eti leo u wabezwa, uozeamo lindini
Fundi mtimba malindi, lindini wajambajamba!


WASIFU WA NTAI WA NKURARU*
Ndo! Ndo! Nadondokwa tozi, hisimuliya wasifu
Na japo ni’twe kilizi, waja wakanikashifu
Silifuti lino tozi, talifuta nili mfu
Ni la Ntai wa Nkuraru, shujaa aletuwata.

Ewe kifo ulo muwi, kiza kisobisha hodi
Mbona ukawata wawi, walafi na wafisadi
Wauwaji na watawi, mbona huwapi miadi
Ukona shujaa Ntai, nd’e bora wa kunyakuwa?

Oi Ntai mwenye haki, mnyonge hamuonei!
Oi Ntai msi chuki, moyoni msi adui!
Oi Ntai stahiki, asenena jambo mbii?
Oi Ntai mbona Ntai, wawi wa chungu nzima?

Humwita Mumeru sugu, wa mlengo wa kushoto
Kwa kuyang’owa magugu, yasiharibu pareto
Wakafanya vuguvugu, kukimbiya mkeketo
Leo Ntai aendile, yupi atayetuponya?

Ntai rafiki wa waja, wakiwa kwa punguwani
Wote kawapa faraja, tajiri kwa masikini
Vitisho hangevitaja, kahubiri tumaini
Ntai mbona iwe wewe, mwalimu mwenye kadiri?

Ntai msomi mkuu, asechoshwa na elimu
Kwani kingi chake kiu, kusaka elimu tamu
Akenda vyuo vikuu, huko ng’ambo piya humu
Kifo kimetupokonya, Ntai msomi mkuu.

Mwenyekiti wa wasomi, akiwa chuo kikuu
Kwenye wongo hasimami, japo kwa vita vikuu
Ya nyuma hayatizami, bali ya mbele na juu
Ndoto ya Ntai jameni, nani ’taifaulisha?

Mwalimu alekiuka, mipaka kuipasua
Hata ng’ambo akavuka, wazungu kuwakosoa
Siasa iso mataka, nd’o Ntai kahubiria
Pengo la Ntai naliya, kulijaza hiwezeki!

Biashara ya miraa, aipelekele ng’ambo
Yake iso umang’aa, biashara iso kombo
Ulaya walimjua, hauzi miraa shombo
Mbona kifo kachagua, Ntai asiye haramu?

Tamati nafunga wimbo, wasifu wa Wa Nkuraru
Hakuna asiye kombo, aishiye ja kunguru
Walau dunia shombo, tuishipo tushukuru
Mola amlaze pema, shujaa Ntai Nkuraru.

*Marehemu Ntai wa Nkuraru alikuwa mwalimu, mfanyi biashara na
mwanasiasa wa upinzani kutoka Nyambene (Meru kaskazini), Kenya.
Alipofariki akiwa katika ziara ya kibiashara mjini London, Uingereza,
mnamo 1998, kifo chake kilizua shuku kwamba aliuawa kwa kurogwa
na wafanyi biashara washindani ama wapinzani wake wa kisiasa.
Mwandishi aliwahi kukutana naye mara moja huko Meru.


YAJAPO YANGU MAUTI
Hakika mawi mauti, usingizi ughasio
Huyafikisha tamati, maisha na utamuo
Mauti nayo sharuti, ndo mwisho wa safario
E Mola nipa hekima, yajapo niwe tayari.

Yajapo yasinipate, mtimangu una kiza
Usafishe utakate, kizani ’pate angaza
Madhambi yasinitate, anasa kunipumbaza
E Mola nipa hekima, yajapo niwe tayari.

Yajapo yangu mauti, siku yangu ifikapo
Nipa onyo la tamati, kunilaza utakapo
Niazime burangeti, usingizi ujiripo
E Mola nipa hekima, yajapo niwe tayari.

Yajapo niwe tayari, ghafula yasinijiye
Ndipo wangu utajiri, wanangu niwagawiye
Tikiti ya kuabiri, hakate nisikawiye
E Mola nipa hekima, yajapo niwe tayari.

Ninatamatisha duwa, kwa Mola wangu Muweza
Ndipo uneni natuwa, ewe Mola niongoza
Yajapo nipate juwa, mauti yenyi kuliza
E Mola nipa hekima, yajapo niwe tayari.

***


Want to review or comment on this book?
Click here to login!


Need a FREE Reader Membership?
Click here for your Membership!Reader Reviews for "Pepo Nne: Diwani ya Malenga wa Mlima Meru"

Reviewed by Mwiti M'Marete 5/14/2014
<a href="http://www.lulu.com/commerce/index.php?fBuyContent=7609881"> <img src="http://static.lulu.com/images/services/buy_now_buttons/en/book.gif?20140501080755" border="0" alt="Support independent publishing: Buy this book on Lulu."> </a>

Popular Poetry Books
  1. Heart & Soul
  2. Through the Mist
  3. Poems of Love & Spirit
  4. Glimpses
  5. Glimpses
  6. Carrboro Poetica
  7. Whispers in the Wake
  8. Sublime Planet, A Chapbook Celebrating the
  9. Perceptions
  10. Facing each day

On Trains by Linda LeBlanc

Literary,accessible lyrics and narratives with universal appeal..  
BookAds by Silver, Gold and Platinum Members

Authors alphabetically: A B C D E F G H I J K L M N O P Q R S T U V W X Y Z

Featured Authors | New to AuthorsDen? | Add AuthorsDen to your Site
Share AD with your friends | Need Help? | About us


Problem with this page?   Report it to AuthorsDen
© AuthorsDen, Inc. All rights reserved.